Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza katika Chemba ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa siku moja wa Baraza hilo uliofanyika juzi ( jumatatu) mkutano huo ulihusu mageuzi ya sekta za usalama, ambapo kwa mara ya kwanza Baraza Kuu la Usalama lilipitisha Azimio linalojitegemea kuhusu mageuzi katika sekta za usalama. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 42 zilizochangia majadiliano hayo yaliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ambapo hoja iliyozungumzwa na wengi ni umuhimu wa nchi kumiliki mchakato wa mageuzi ya sekta za usalama. Nyuma ya Balozi, ni Lt. Kanali Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi katika Uwakilishi wa Kudumu
Na Mwandishi Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeungana na mataifa mengine katika kusisitiza umuhimu wa nchi kumiliki mchakato wa Mageuzi ya Sekta za Usalama ( Security Sector Reform)
Akichangia majadiliano ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikutaka kwa siku nzima ya jumatatu kujadili taarifa ya Katibu Mkuu kuhusu SSR. Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katikak UN, Balozi Ramadhan Mwinyi amesema, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi inapenda kuona kwamba mageuzi ya sekta za usalama yanamilikiwa nan chi zenyewe zikiwamo nchi zinazotoka katika machafuko.
Katika Mkutano huo wa jumatatu, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha kwa kauli moja na kwa mara ya kwanza Azimio linalojitegemea kuhusu mchakato wa Mageuzi ya Sekta za Usalama.
Kupitia azimio hilo namba 2151 (2014) pamoja na kusisitiza umuhimu wa dhana zima ya mageuzi ya sekta za usalama na umuhimu wake kwa usalama, amani na ustawi wa mwanadamu. Azimio linasisitiza kwamba umiliki wa nchi katika mageuzi hayo ni jambo la muhimu
Akaongeza kuwa makundi ya wapiganaji na ambao wameka silaha zao chini na kuingia katika mchakato wa majadiliano wanapashwa pia kuwa sehemu ya mageuzi ya sekta za usalama.
Akasema kwa kuyashirikisha makundi hayo ya wapiganaji na mengine kutasaidia ujenzi wa Amani na usalama na pia kuepusha kujirudia kwa mapigano.
Aidha Balozi Mwinyi, ameleza kwamba, nchi zinazopakana na nchi zinazotoka kwenye machafuko pia zinayonafasi na wajibu wakutoa ushirikiano na uzoefu wao katika ujenzi wa sekta za usalama.
Vile vile Balozi amebainisha kwamba katika miongo ya miaka mitano iliyopita imedhihirisha wazi umuhimu wa jumuia za kikanda katika uzuiaji wa mapigano, ulinzi wa Amani na ujenzi wa Amani.
Majadiliano hayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na yaliitishwa na Nigeria ambayo ni Rais wa Baraza hilo kwa Mwezi huu wa April. Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Bw. Aminu Wali aliongoza majadiliano.
Wawakilishi kutoka nchi 42 wanachama wa Umoja wa Mataifa, zilizungumza wakati wa majadiliano kuhusu dhana hiyo ya mageuzi ya sekta za usalama, na bila ya kujali tofauti zao, kila moja ilisisitiza hoja ya nchi kumiliki mchakato huo hata kwa zile ambazo zimetoka katika machafuko au mapigano.
Aidha pamoja na kusisitiza haja na umuhimu wa nchi kumiliki mchakato huo, zimeongeza kuwa bado kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa, kuziwezesha nchi hasa zile zinazotoka katika machafuko kuweza si kujenga upya sekta hizo za usalama bali pia kuzifanyia mageuzi.
Vile vile ilielezwa ilisisitizwa pia kuwa mageuzi hayo ya sekta za usalama ni muhumu katika kuziimarisha nchi ambazo ndiyo kwanza zimetoka kwenye machafuko. Na kwamba mageuzi hayo yatapewa kipaumbele katika utekelezaji mamlaka za ulinzi wa Amani na misheni za maalum za Kisiasa
Wajumbe wengine walikwenda mbali zaidi, kwa kueleza kwamba mageuzi hayo ya sektza za usalama yanapashwa kuwa jumuishi kwa maana ya kushirikisha makundi mengine ya kijamii. Lakini kwa msisitizo kwamba serikali ndiyo iwe na mamlaka ya kuamua mfumo wa sekta zake za usalama.
Katika salamu zake za ufunguzi Ban ki Moon, alisema, lengo la kutekeleza mageuzi ya sekta za usalama ambazo ni pamoja na jeshi, polisi na vyombo ya usalama ni kuwawezesha wananchi ambao ndiyo walengwa kuisha maisha yenye usalama.
“Sekta za Usalama ndiyo muhimili mkuu wa makubaliano kati ya serikali na wananchi wake. Mamlaka ya kutumia nguvu ni lazima yaendane na wajibu wa kulinda raia na kuheshimu haki za binadamu” akasema Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa Ban Ki Moon, sekta za usalama zinazotekeleza majukumu yake chini ya misigi ya utawala wa sheria zinauwezo wa kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao na hivyo kuchangia katika uimara wa ujenzi wa Amani na maendeleo.