Quantcast
Channel: VIJIMAMBO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 45918

UCHAGUZI KALENGA: Mbowe: Nitafia angani

$
0
0
  Inafuatia polisi kupiga marufuku chopa kuruka kesho
  NEC: Ruksa endapo hazina nembo, alama ya chama
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
 
Wakati Polisi mkoani Iringa imepiga marufuku helikopta za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, unaotarajiwa kufanyika kesho, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe amesema yupo tayari kufa angani.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa kuhusu hali ya usalama na polisi walivyojipanga kukabiliana na matukio ya vurugu yanayotishia uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi huo.
 
 Alisema kuwa hakuna chama chochote cha siasa kinachoruhusiwa kurusha helikopta angani siku ya Jumapili kwa kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ambazo kisheria NEC imeweka ukomo ambao ni Machi 15, saa 12:00 jioni.
 
Mungi alisema chama ambacho kitarusha helikopta hizo kwa kisingizio cha kulinda kura zao ni kuvunja sheria kwa kuwa kura hizo zinalindwa na mawakala waliotajwa kwenye sheria ya uchaguzi.
 
MBOWE: NIPO TAYARI KUFIA ANGANI
Mbowe, akizungumza katika mkutano wa kampeni kijiji cha Sadani, alisema kauli ya kamanda wa polisi Iringa kuzuia chopa yao ni mkakati wa kutaka kusababisha maafa na yupo tayari kufia angani siku ya Jumapili.
 
"Tutaruka kwa chopa mbili, RPC Mungi apende asipende niko tayari kufa...Nazungumza kwa mamlaka kama kiongozi mwenye dhamana. Nchi hii kila mtu ana haki ya kutumia usafiri wowote...Hatutaogopa kuruka kwa chopa, mpeni salam kamanda wa polisi," alisema Mbowe.
 
NEC YATOA UFAFANUZI
 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, akizungumzia matumizi ya chopa yaliyotangazwa na Chadema, alisema kuwa chombo chochote ambacho kilitumika katika kampeni hizo, kikiwa na nembo au bango la chama chochote cha kisiasa hakitakiwi kwenye uchaguzi huo, isipokuwa kama vitaondolewa vitu hivyo, vinaruhusiwa kutumika.
 
"Tunachosisitiza hapa ni material (nyenzo) ambazo zilikuwa zikitumiwa wakati wa kampeni na hatuhitaji kuona nguo, kofia wala magwanda siku hiyo...Matumizi ya chopa sisi kama tume, hatujakataa kutumika lakini tunasema kama itatumika kubeba abiria kutoka uwanja fulani kwenda sehemu nyingine na si kutua kwenye kituo cha kupigia kura, hapo ni sawa,"alisema Jaji Lubuva.
 
Alisema ni vigumu NEC kuijibia polisi kuhusu katazo la matumizi ya helikopta hizo siku ya uchaguzi lakini ukweli ni kwamba kama wataweza kutofautisha mambo waliyokuwa wakiyafanya katika kampeni zao na uchaguzi huo, wanaweza kuitumia.
 
Hata hivyo, Meneja kampeni za Chadema jimbo la Kalenga, Godbless Lema, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, alisema chopa ya Chadema inayomilikiwa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, itapasua anga kama kawaida ikiwa imembeba mgombea wao, Grace Tendega na viongozi wengine wa chama hicho.
 
"Tutaitumia helikopta yetu kusambaza chakula na maji kwa mawakala wetu katika vituo 216 vilivyotengwa. Helikopta ni usafiri kama gari ambalo wanatumia CCM au Chadema katika kampeni hizi...CCM wana magari yao ambayo ni Land Cruizer na Chadema tunazo Ford Ranger halafu yameruhusiwa kutumika lakini chopa hawataki; kwani nani asiyejua lipi ni la nani,"alihoji Lema.
 
Alisema Chadema itaheshimu sheria za uchaguzi kwa kuondoa nembo na alama za kichama katika helikopta hiyo na kuitumia kufanya kazi muhimu ikiwamo kumsaidia mgombea kuvifikia vituo vilivyopo mbali katika jimbo hilo.
 
Alisema hata kama vyombo vya dola vinakazana kuzuia matumizi hayo ya helikopta, Chadema pia imejipanga kuzuia uhalifu wowote katika jimbo hilo lakini pia wanategemea kuongeza idadi ya vijana wengine 1,000, watakaongeza nguvu kwenye kata zote 13.
 
DAFTARI LA WAPIGA KURA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni na Oganaizesheni za Chadema, Benson Kigaila alisema NEC inajaribu kuficha ukweli kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa sababu imeongeza kinyemela majina ya watu zaidi ya 1,000 katika daftari la wapiga kura bila ya kutangaza kwa umma na kuvishirikisha vyama shiriki katika uchaguzi huo.
 
"Kwa nini daftari hili liboreshwe Kalenga tu, halafu wasitangaze umma ukajua au kuvishirikisha vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu. Huku kuna maanisha nini kama si hujuma lakini pia hadi jana kuna mawakala zaidi ya nusu walikuwa hawajaapishwa,"Alisema Kigaila.
 
Alisema kufuatia ucheleweshaji huo, mawakala wao kama watakuwa hawajaapishwa hadi Jumamosi, Chadema kinaitaka Tume ya Jaji Lubuva kuwaapisha wakiwa kwenye vituo vyao kwa sababu hawatakubali kama chama vituo hivyo vikabaki wazi kwa minajili ya kusubiri mihuri.
 
CHANZO: NIPASHE

Viewing all articles
Browse latest Browse all 45918

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>