Quantcast
Channel: VIJIMAMBO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 45981

Kishindo kikuu chasubiriwa leo

$
0
0
 Wengi wataka hotuba ya JK itulize upepo mbaya
Ile hofu ya kuviziana na mbinu za kuteka Bunge Maalum la Katiba, leo ama itaendelea kutawala mchakato wa kutunga katiba hiyo au utafikia mwisho kutegemeana na maudhui ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete,atakayowasilisha bungeni mjini hapa leo.

Rais Kikwete atahutubia Bunge hilo leo likiwa tayari kwa kuanza kazi ya kuchambua Rasimu ya Katiba ambayo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, Jumanne wiki hii ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Muungano wa Tanzania aliweka wazi mambo ambayo yamekwaza muundo wake na kufafanua majaribu ya miaka 30 ya kutaka kuuanzishwa kwa muundo wa serikali tatu ambao alisema haukwepeki kwa sasa.

Msimamo wa Tume ya Mabadilko ya Katiba juu ya serikali tatu unapingwa kwa nguvu zote na CCM ambayo imekwisha kuandaa waraka maalumu wenye mambo manane kusisitiza ni kwa nini serikali mbili bado ni bora zaidi katika kuenzi Muungano.

Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia Bunge hilo kwa mujibu wa kanuni ya 75 ya Bunge hilo, hotuba ambayo inatarajiwa kujibu baadhi ya maswali ambayo wajumbe ama wamekuwa wakiulizana au kutuhumiana juu ya mustakabali wa katiba mpya hoja ikijengwa kwamba kuna njama za vyama za kutaka kuteka mchakato huo, CCM ikituhumiwa zaidi.

Watanzania wanasubiri kwa hamu kubwa kusikia atakachokizungumzia Rais Kikwete kuhusu mchakato wa katiba mpya, wakikumbuka juhudi zake binafsi ambazo zilifanikisha kukwamua mkwamo wa mchakato huo mara mbili katika hatua ya kutunga sheria Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2012.

Baadhi ya watu wanaobashiri kuwa huenda Rais Kikwete atajibu hatuba ya mambo aliyoyazungumza Jaji Warioba kutetea muundo wa serikali tatu na wengine wakitabiri kwamba huenda atajielekeza kusaka maridhiano miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo ambao wamegawanyika kimtazamano na kiitikadi.

Miongoni mwa mambo ambayo yamewagawa ni suala la muundo wa Muungano kutokana na wajumbe kutoka CCM kwenda na msimamo wa kutetea serikali mbili na vyama vingine na baadhi ya wajumbe kutoka asasi na makundi kutetea serikali tatu.

Suala lingine lililosababisha tofauti ni kanuni ya 37 na 38 kuhusu maamuzi ya kupitisha katiba kutolewa kwa utaratibu wa kura ya siri au wazi.

Kutokana na suala la muundo wa Muungano kuteka mjadala tangu rasimu ya kwanza ya katiba ilipotolewa ikipendekeza serikali tatu, huenda Rais Kikwete akatumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuzungumzia jambo hilo kuliko mambo mengine.

Mambo mengine ambayo CCM inaonekana kutokuwa tayari kuyaunga mkono, ni kupunguzwa sana kwa madaraka ya Rais, hususani katika uteuzi wa baadhi ya viongozi waandamizi kwa kuthibitishwa na Bunge baada ya kuteuliwa na wengine majina yao yapendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma kabla ya uteuzi.

Suala lingine ni la mawaziri kutokuwa wabunge, wabunge kutokuwa mawaziri, ili kulipa Bunge madaraka ya kuisimamia serikali sawasawa.

Eneo jingine linaloamsha ubishi wenye sura ya itikadi ya vyama ni juu kuwapo kwa ukomo kwa wabunge kwa kuwawekea vipindi vitatu vya miaka mitano kila kimoja.

Rasimu pia inapendekeza wananchi kumwondoa madarakani mbunge wao anaposhindwa kuwajibika kwao tofauti na ilivyo sasa kwa mbunge kukaa madarakani kwa miaka mitano hata kama hawajibiki kwa wapigakura wake.

Hakuna mwenye uhakika kuhusu maudhui ya hotuba ya Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Dodoma jana, lakini kualikwa kwa viongozi wote wa kitaifa walioo madarakani na wastaafu kumsikiliza kunatoa hisia kwamba hituba hiyo ni ya kuweka mambo sawa kabla ya wabunge kuanza rasmi kazi ya kuchambua Rasimu ya Katiba ambayo iliwasilishwa bungeni Jumanne wiki hii.

MATARAJIO YA WAJUMBE
Wabunge wa Bunge hilo wamesema wanatarajia hotuba ya Rais Kikwete itasaidia ‘kusafisha’ hali ya hewa kwa kuondoa mivutano iliyopo ili wote waungane na kuwa kitu kimoja katika suala la kutunga katiba kwa maslahi ya taifa.

SALEHE
Salehe Mohamed Salehe kutoka miongoni mwa wabunge 201 anayewakilisha wakulima kutoka Zanzibar, alisema atarajia Rais atoe nasaha na usahuri mzuri kwa wabunge ili kazi ya kutunga katiba ifanyike kwa amani na utulivu.

“Natarajia Rais atoe nasaha juu ya mwenendo wa Bunge linavyoendelea, atoe maelekezo na ushauri ili lengo la wananchi kupata katiba bora litimie,” alisema Salehe.

AKSON
Dk. Tulia Akson, mwakilishi wa Taasisi ya Elimu, alisema kuwa matarajio yake kwenye hotuba ya Rais ni kuona akiwaunganisha wajumbe na Watanzania kwa ujumla ili washikamane katika kuhakikisha wanakubaliana na kupata katiba nzuri. Alisema kwa jinsi hali ilivyo sasa kuna mgawanyiko wa wazi baina ya wanasiasa wenye misimamo tofauti, hali ambayo inafanya mijadala ya Bunge hilo kutawaliwa na malumbano yasiyokuwa na tija.

MATIKO
Ester Matiko ni kutoka Chadema, alisema atarajia hotuba ya Rais itajikita katika kufanikisha upatikanaji wa katiba na siyo kutetea misimo ya CCM.

“Tunatambua kuwa Rais ndiye mwenyekiti wa CCM, lakini tunatarajia kuwa anakuja hapa bungeni kama Taasisi, aje aongee kama Rais na siyo kama Mwenyekiti wa CCM, ijikite katika kuzungumzia mafanikio ya kupata katiba mpya na siyo mtazamo wa chama chake,” alisema Matiko.

Alisema kuwa hatarajii kumsikia Rais akija kujibu hoja za Jaji Warioba kwa madai kuwa akifanya hivyo atakuwa anakwaza watu wengi akiwamo yeye.

NGOYE
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Hilda Ngoye, alisema anatarajia kuwa Rais Kikwete atatoa hotuba nzuri ya kuwajengea Watanzania matumaini ya kupata katiba nzuri na iliyo bora.

“Natarajia kesho (leo) Rais atatujengea matumaini, atatupa moyo ili tuendelee vizuri na mchakato huu wa katiba ili hatimaye tuumalize kwa amani tukiwa na katiba nzuri inayojali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Ngoye.

Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, Dodoma na Thobias Mwanakatwe, Dar

Viewing all articles
Browse latest Browse all 45981

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>