Quantcast
Channel: VIJIMAMBO
Viewing all articles
Browse latest Browse all 45981

Siasa za udugu, urafiki zinavyoshika kasi nchini

$
0
0
Uongozi ni hali ya kushawishi kundi kutekeleza malengo fulani waliyojiwekea. Kuna aina nyingi za uongozi kulingana na jinsi wanavyopatikana.
Kuna uongozi wa kuteuliwa, kuchaguliwa kidemokrasia, kurithishwa (wafalme) na uongozi wa kipaji.
Hata hivyo, kumekuwa na tabia ya viongozi kurithisha madaraka kwa ndugu na jamaa zao kwa lengo la kulinda masilahi ya kifamilia yasipotee wakati hawapo madarakani.
Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejikuta kikirejesha watoto wa viongozi katika nafasi za ubunge pale nafasi inapokuwa wazi, huku vyama vya upinzani navyo vikiendelea na mtindo huo hali inayoonyesha uroho wa madaraka. 
Hivi karibuni CCM kimemsimamisha Godfrey Mgimwa ambaye ni mtoto wa Dk William Mgimwa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenga kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Godfrey Mgimwa alishinda kura za maoni kwa kupata 342, huku mshindi wa pili, Jackson Kiswaga akipata kura 170, watatu ni Hafsa Mtasiwa aliyeambulia kura 42.
Katika uchaguzi huo, Mgimwa anapambana na Grace Tendega wa Chadema.
Akijibu shutuma kwamba, jimbo hilo linarithishwa kifamilia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema chama hicho hakiwezi kumnyima mwanachama yeyote haki ya kuwania kwa sababu tu wazazi wake waliwahi kuwa viongozi.
“CCM haiwezi kumzuia Godfey kuwania eti kwa sababu ni mtoto wa Dk Mgimwa (marehemu). Yeye ana haki ya kuwania kama watu wengine tunachoangalia ni uwezo wake na hilo limeonyeshwa baada ya wananchi wa Kalenga kumpa ushindi wa kishindo,” alisema.
Wakati joto la uchaguzi likishika kasi  Kalenga, jimbo la Chalinze mkoani Pwani nako amepitishwa mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani. CCM imempitisha Ridhiwani baada ya kushida kwa kura 758, akifuatiwa na Wakili Imani Madega aliyepata kura 335.
Mbali na wagombea hao wapya,  mwaka 2012 baada ya kufariki aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari ambaye pia alikuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, CCM ilimsimamisha mwanaye, Sioyi Sumari kugombea.
Hata hivyo mgombea wa Chadema,  Joshua Nasari alishinda
Mbali na ubunge, mwaka 2000 chama hicho kilishamrithisha madaraka ya urais  Amani Abeid Karume  mtoto wa mwasisi wa Taifa la Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Amani alikuwa rais wa sita wa Zanzibar, huku ndugu yake, Ali Karume naye akiiwania nafasi hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio.
Hali hiyo ya kurithishana madaraka iwe kwa kuteuliwa au kupendekezwa kugombewa haipo CCM pekee, bali hata kwa vyama vya upinzani.
 C hadema: Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya chini kwa chini juu ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye ni mkwe wa mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Mbowe amekuwa mwenyekiti wa chama hicho tangu mwaka 2004 alipogombea na kushinda akimrithi Bob Makani (marehemu).
Katika uchaguzi mkuu wa chama hicho wa 2009, wazee wa chama hicho wakiongozwa na Mtei, walimzuia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kugombea nafasi hiyo kwa maelezo kuwa hajakomaa, huku wakimtaka amwachie Mbowe amalizie kipindi chake cha pili.
Mwaka huu,  Chadema itafanya uchaguzi mkuu, lakini haijaeleweka kama Mbowe ataendelea kugombea nafasi hiyo au atamwachia mwingine.
Undugu katika Chadema umeonekana kushika kasi katika nafasi za ubunge wa kuteuliwa ambapo ndugu wa kifamilia wa viongozi wa juu wanaonekana kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalumu.
Lucy Owenya aliyepata ubunge wa viti maalumu kwa kipindi cha pili sasa ni mtoto wa moja wa waasisi, kiongozi  wa chama hicho na mbunge wa Moshi mjini Philemon Ndesamburo.
Wengine ambao ni wabunge wa viti maalumu na ambao ni ndugu wa karibu wa viongozi wa juu wa chama hicho ni pamoja na Grace Kiwelu aliyedumu katika ubunge wa viti maalumu kwa vipindi vitatu, ambaye ni mke wa mtoto wa Ndesamburo na Rose Kamili  alikuwa mke wa Katibu Mkuu Dk Wilbroad Slaa .
Undugu pia unatajwa kudhoofisha demokrasia ndani ya vyama vya siasa ikiwamo UDP ambako mwenyekiti wake,  John Momose Cheyo na mdogo wake, Isaack Cheyo wamekaimishana uongozi wa chama hicho.
Chanzo;mwananchi

Viewing all articles
Browse latest Browse all 45981

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>